Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Muhina Seif Mohamed Kaduguda amewatoa hofu Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, kuhusu uhalali wa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison anayehusishwa kujiunga na Young Africans.
Morrison anatajwa kusaini Young Africans katika kipindi hiki ambacho mkataba wake na Simba SC unaelekea ukingoni, jambo ambalo limewashtua Mashabik na Wanachama wa klabu hiyo ya Msimbazi.
Kaduguda amezungumza na Dar24 Media na kueleza kuwa, bado anafahamu Kiungo huyo ni mchezaji halali wa klabu ya Simba SC, na jukumu la kusema atabaki ama kuondoka mwishoni mwa msimu huu lipo chini Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez.
“Tumeshatoka huko msiturudishe nyuma, Simba SC imeshakua klabu kubwa kwa mujibu wa zile kanuni tano za Shirikisho la soka la Dunia ‘FIFA’ na Shirikisho la Soka la Afrika ‘CAF’, moja ya utaratibu wa kuwa klabu kubwa ni kuwa na utaratibu wa utawala Bora, sisi tuna msemaji wetu tunamlipa pesa kwa ajili ya kuangalia ofisi,maslahi ya wachezaji, maslahi ya timu na kila kitu.”
“Morrison yupo Simba SC na bado tunajua ni mchezaji wetu, sasa kama kuna jambo lingine lolote kuhusiana na Morrison, basi Barbara atasema.”
Kaduguda pia akazungumzia sakata la Kiungo Clatous Chotta Chama kwa kusema: “Sijasikia chochote, Chama ni mchezaji wa Simba SC na Pablo ni Kocha wa Simba SC, hizi Blabla ndio maana ninasema Simba SC tumeshavuka huko, hatupo tena huko.”