Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba Mwina Kaduguda amesema klabu hiyo haijashtushwa kwa lolote kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa Msemaji wao Haji Manara.
Kaduguda amesema Simba SC ipo imara na itaendelea kuwa imara zaidi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu kutokana na mipango waliojiwekea ambayo haiwezi kutetereshwa na kuondoka kwa mtu ambaye amefanya maamuzi yake binafsi.
Kiongozi huyo amesema ikitokea Muwekezaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo Mohamed Dewji ‘Mo’ akaondoka, ndio Simba SC itayumba kwa sababu ameshikilia muhimili wa klabu.
“Sisi Simba tutashtuka endapo akiondoka Mohamed Dewji, kwa sababu ni mtu mwenye mashiko na klabu hii, sio mtu mwingine ambaye alikua wakawaida sana.” amesema Kaduguda.
Kuhusu tamasha la Simba Day Kaduguda amesema tamasha hilo litafanyika kama kawaida, huku akiwataka Mashabiki na Wanachama kupuuza taarifa za kubumba.
“Nasema hivi, Simba Day iko pale pale, huu ni ustaarabu wa Simba ambao ulianzishwa makusudi kwa ajili ya wanasimba, kwa nini tusiufanye kama kawaida yetu?”
“Nawaomba Mashabiki na Wanachama wapuuze taarifa za kubumba huko mtaani ambazo zinadai Simba Day haitakuwepo kwa mwaka huu.” amesema Kaduguda.
Hata hivyo mpaka sasa uongozi wa Simba SC haujatangaza tarehe maalum ya kufanyika kwa Tamasha la Simba Day, huku watani zao wa jadi Young Africans wakitarajia kufanya Tamasha lao la Siku ya Mwananchi Jumapili (Agosti 29) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.