Klabu ya Simba SC ipo tayari kufanya Uchaguzi Mkuu wa Viongozi upande wa Wanachama ambao wataamua nani atakwenda kuwawakilisha kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu hiyo.
Simba SC kwa sasa inongozwa na Mwenyekiti Multaza Mangungu ambaye alichaguliwa kuziba nafasi ilioachwa wazi na Swedi Nkwabi ambaye aliamua kujiuzulu mwaka mmoja, baada ya kuchaguliwa na Wanachama.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye ni sehemu ya viongozi waliopatikana kupitia Uchaguzi Mkuu wa miaka minne iliyopita, Mwina Seif Mohamed Kaduguda, amethibitisha kuwa Mchakato Uchaguzi Mkuu wa Simba SC upo tayari na wakati wowote utatangazwa hadharani na Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzales.
Kaduguda ameweka wazi harakati hizo za Uchaguzi alipohojiwa na Kituo cha Radio cha EFM, huku akisema hakutakua na danadana.
“Uchaguzi wa Simba SC hauna danadana. Tarehe ya Uchaguzi imeshapangwa na Mtendaji Mkuu wa klabu Barbara Gonzales atakuja kuutangaza. Mimi sio msemaji katika hili, lakini jua Uchaguzi uko na utakuja kutangazwa.”
“Kwa sasa Barbara yuko Qatar kwenye Fainali za Kombe la Dunia, amekwenda huko kwa ajili ya kujifunza vitu mbalimbali vya kuifanya Simba SC izidi kwenda juu. Uzuri Wanasimba hawana tatizo na Uchaguzi wao.” amesema Mwina Kaduguda
Tangu Simba SC ilipoingia katika Mfumo wa Mabadiliko ya Kiutendaji, imekua ikiendeshwa kwa mfumo wa Uongozi kutoka kwa Mwekezaji na sehemu nyingine inatoka kwa Wanachama, ili kuunda Bodi ya Wakurugenzi ambayo hufanya maamuzi ya Kimaendeleo ya Klabu hiyo.