Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila ameutaka mpango kazi wa kuratibu taasisi na mashirika yanayotoa msaada wa kisheria kwa wananchi ukamailike haraka ili wananchi wapate huduma ya usaidizi wa kisheria kwa ufanisi.
Ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha wadau wa msaada wa kisheria kwa Mikoa ya Nyanda za juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa na Songwe.
“Watu wengi wamepoteza haki zao kwa kutokujua sheria au kutokuwa na fedha za kumudu gharama za mawakili lakini serikali imetengeneza utaratibu wa kuratibu taasisi ambazo zinatoa msaada wa kisheria bila malipo ili wananchi wengi zaidi wasiojiweza waweze kupata msaada wa kisheria na wasikose haki zao,” amesema Kafulila.
Amesema kuwa mpango kazi wa kuziratibu taasisi zinazotoa msaada wa kisheria uwe unapimika na hasa uwe na lengo la kutoa elimu kwa wananchi ili wajue kuwa hata kama hawana fedha za kugharimia mawakili wa kuwatetea ili wapate haki zao.
Naye Msajili wa Mashirika na taasisi zinazotoa Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Felista Joseph amesema kuwa elimu kwa umma itapewa kipaumbele katika mpango kazi huo na ni jambo la msingi ili wananchi wafahamu uwepo wa taasisi hizo
Kwa upande wake Mratibu wa shirika la Gender and Social Reform, Steward Shiwuga amesema shirika lake limekuwa likipata vikwazo katika kutoa msaada wa kisheria bila gharama yoyote na pia baadhi ya watendaji wamekuwa hawatoi ushirikiano kwao.
Msajili Msaidizi wa Taasisi za Msaada wa kisheria kwa Wilaya ya Ileje, Rodrick Sengela amesema kuwa hapo awali taasisi hizo zilijiendesha bila kuratibiwa pia baadhi ya watu wasio waaminifu walikuwa wakiwarubuni wananchi na kuwatoza fedha nyingi pale wanapohitaji msaada wa kisheria lakini kwa sasa wananchi wataelimisha mahali sahihi pa kupata msaada wa kisheria bila malipo.