Rais wa Rwanda, Paul Kagame leo amepitishwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Kagame amepitishwa katika Mkutano wa 20 wa Jumuiya hiyo uliofanyika jijini Arusha uliohudhuriwa na wakuu wa nchi wanachama na viongozi wengine waliowawakilisha wakuu wa nchi zao.

Mwenyekiti huyo amezitaka nchi wanachama kuhakikisha Jumuiya hiyo inakuwa na jamii bora kwani maendeleo hupimwa kwa idadi ya watu waliofanikiwa kutokana na program za nchi hizo.

Amesema kuwa yeye atajikita zaidi katika uboreshwaji wa miundombinu, upatikanaji wa huduma bora za afya pamoja na kuimarisha mfumo wa ulinzi mipakani ili kupambana na tishio la ugaidi.

Kwa upande wa mtangulizi wake, Rais Museveni amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imepiga hatua nzuri katika kuboresha ushirikiano na uchumi wa ukanda huo. Aliongeza kuwa, Jumuiya hiyo bado inapaswa kuchukua hatua stahiki katika kuongeza kasi ya miundombinu ya kuunganisha eneo hilo na kuwapunguzia wananchi gharama za umeme.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alikuwa mwenyeji wa viongozi wenzake katika Mkutano huo wa 20. Marais waliohudhuria ni pamoja na Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda) na Uhuru Kenyatta (Kenya). Rais Pierre Nkurunzinza (Burundi) amewakilishwa na Makamu wake wa kwanza; na Rais Salva Kiir (Sudan Kusini) ambaye ni mualikwa pia akiwakilishwa na Waziri wa Biashara, Paul Mayon.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 2, 2019
Mahakama yawaachia huru watuhumiwa wa ugaidi Kenya