Rais wa Rwanda, Paul Kagame amesema kuwa amefanya mazungumzo na Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu mapambano dhidi ya virusi vya corona (covid-19).
Kagame ametumia mtandao Twitter kuelezea kwa ufupi mazungumzo hayo, akisema yamekuwa yalikuwa mazuri.
“Nimekuwa na mazungumzo mazuri na Rais Donald Trump. Tumezungumzia uhusiano wetu mzuri, na jinsi anavyotuunga mkono yeye binafsi, na utawala wake unaifikia Rwanda katika kupambana na mlipuko wa covid-19. Tunathamini sana,” tafsiri isiyo rasmi ya Tweet ya Rais Kagame.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Serikali ya Marekani kuongeza msaada wa kifedha kiasi cha $4 milioni, kuisaidia sekta ya afya ya Rwanda.
Ubalozi wa Marekani nchini Rwanda, jana, Aprili 24, 2020 ulisema kuwa nyongeza ya fedha kwa Rwand itaongeza uwezo wa Serikali ya nchi hiyo katika kupambana na maambukizi ya covid-19.
Hadi jana, Aprili 24, 2020 kulikuwa na jumla ya visa 176 vilivyoripotiwa nchini Rwanda, wagonjwa 87 wakipata nafuu na kwa bahati nzuri hakuna vifo.