Idadi ya watoto waliopoteza maisha kutokana na tukio la bweni la Shule ya Msingi ya Kiislamu ya Byamungu wilayani Kyerwa mkoani Kagera kuteketea kwa moto imeongezeka, baada ya mtoto mmoja kati ya wanne waliokuwa wanapatiwa matibabu hospitalini kufariki dunia.

Tukio hilo la bweni kuteketea kwa moto lilitokea Septemba 14, 2020 majira ya usiku na kusababisha vifo vya watoto 10 wenye umri kati ya miaka minne (4) na kumi na mbili (12).

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyerwa, Benjamin Mwikasyete amekaririwa na Daily News akieleza kuwa mtoto huyo aliyekuwa miongoni mwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza alifariki dunia Jumatatu usiku.

Alimtaja mtoto huyo kuwa ni Juma Seif mwenye umri wa miaka saba (7), ambaye alitarajiwa kuzikwa Jumanne kijijini kwao Nkwenda, Kyerwa.

Watoto wanne kati ya watoto sita waliokuwa wamejeruhiwa kwa moto katika tukio hilo walipelekwa katika Hopitali ya Bugando kwa ajili ya matibabu.

Aliwataja watoto wengine watatu wanaoendelea kupatiwa matibabu na majina yao kwenye mabano kuwa ni Lookman Salihina(6), Avitus Sperius (4) na Furaha Ashraf (10).

Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika mkoa wa Kagera, Septemba 16, 2020 Rais John Magufuli aliagiza uchunguzi wa kina ufanyike kubaini chanzo cha tukio hilo.

“Matukio ya moto hayawezi kuruhusiwa kuendelea kuchukua maisha ya watoto wasio na hatia. Viongozi wanapaswa kuchukua hatua ya kuchunguza shule hususan za bweni, na kuhakikisha kuwa mifumo ya kuzuia moto au kutoa tahadhari (fire alert systems) iliyopo onafanya kazi ipasavyo,” alisema Rais Magufuli.

Naye Inspecta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro aliyetembelea eneo la tukio alisema kuwa hakuna kitakachoachwa hadi chanzo cha moto huo kitakapobainika.

IGP Sirro alisema kuwa uchunguzi wa awali ulibaini kuwa moto ulianza katika bweni la wanafunzi wa kiume usiku wa manani, ambapo watoto 74 walikuwa wamelala.

Lissu aahidi neema kwa wakulima Kagera
Kiongozi wa waasi ashinda uchaguzi wa urais