Benchi la Ufundi la Kagera Sugar linatarajiwa kupitisha panga la kuwafyeka baadhi ya wachezaji wasio na mipango nao na kupitisha orodha ya mashine mpya zinazohitajiwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na ASFC.

Imefahamika kuwa baadhi ya wachezaji kama Meshack Mwamita, Ally Ramadhan ‘Kagawa’, Erick Mwijage na Hamis Kizza ‘Diego’ wamemaliza mikataba na huenda wakawa wa kwanza kupewa ‘Thank You’, lakini maamuzi kamili yapo kwa benchi hilo.

Kocha Msaidizi wa Kagera, Marwa Chambeli amesema baada ya kumaliza msimu waliwasilisha ripoti ya kiufundi kwa uongozi wa timu hiyo ili kuipitia, lakini baada ya kutazama mwenendo wa usajili unavyokwenda benchi la ufundi limeazimia kukutana fasta Mjini Bukoba.

“Sio kama tuko kimya hapana nadhani ndani ya juma moja mambo yatakamilika na mtaanza kuona usajili wetu lazima kuwe na maingizo mapya, tulishapeleka ripoti inafanyiwa kazi,” amesema Chembeli na kuongeza;

“Kwa sasa hatuna kikubwa cha kuwaambia lakini tunakutana leo Ijumaa kuona majina tuliyopendekeza yamefikia wapi na kama tunaowataka wanapatikana na kama hawapo tunafanyaje ili kupata malengo tuliyoyataka, nadhani baada ya hapo ndiyo unaweza kusema unaowaacha.”

Ofisa Habari wa Kagera Sugar, Hamis Mazanzala amesema wataweka wazi majina ya wachezaji wanaoachwa na wanaosajiliwa.

JTK lakusanya damu kuchangia wenye uhitaji
TAZAMA yaanza usafirishaji Mafuta safi ya Dizeli