Uongozi wa klabu ya Kagera Sugar umemjibu Rais wa klabu ya Simba Evance Aveva, kufuatia maamuzi aliyoyatangaza juzi mbele ya waandishi wa habari, kuhusu mpango wa kudai point tatu na mabao matatu mbele ya mahakama ya usuluhishi wa michezo CAS.
Aveva alidai Simba SC haikutendewa haki kutokana na kanuni za ligi kuu kuonyesha walipaswa kuachiwa point tatu na mabao matatu kama ilivyoamriwa na kamati ya saa 72, lakini cha kushangaza kamati ya Sheria, Katiba na hadhi za wachezaji ya TFF ilizirejesha alama na mabao hayo Kagera Sugar.
Mratibu wa kikosi cha Kagera Sugar Mohamed Hussein ameiambia Dar24 kuwa, suala la Simba kutaka kwenda CAS ni haki yao na itakua vyema kutokana na utata uliopo, ambao umekua ukiwachanganya wadau wa soka kuhusu uamuzi wa point tatu na mabao matatu, ambao umewanufaisha wao kama washindi wa mchezo wa mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Amesema wanaamini haki inatafutwa kwa kufuata taratibu na sheria, na waliposikia kauli ya Aveva aliyoitoa juzi walifarijika kutokana na jambo hilo litaendelea kutolewa ufafanuzi zaidi kwa mujibu wa taratibu na kanuni za ligi kuu.
Hata hivyo Mohamed Hussein, amehoji kwa nini Simba wamekua na uchungu na point tatu na mabao matatu, ilihali hawakujitahidi uwanjani siku ya mchezo na badala yake walikubali kufungwa mabao mawili kwa moja.
“Simba wakubali tuliwafunga uwanjani, na hata kama wanakwenda CAS watambue tuliwafunga, jambo ambalo lilikua sahihi kwetu kupata point tatu, na ndio maana tulirejeshewa point zetu na kamati ya Sheria ya TFF,”
“Tunawatakia kila la kheri huko waendapo na tunaamini haki itaendelea kuonekana imetendeka, kutokana na wenzetu kupiga hatua zaidi katika masuala ya maendeleo ya soka, hasa linapokuja suala lenye utata la mchezaji kuonyeshwa kadi.” Amesema Mohamed Hussein.
Simba SC wanasubiri nakala la hukumu iliyotangazwa na kamati ya Sheria, Katiba na hadhi za wachezaji, ili waanze mchakato wa kupeleka malalamiko yao CAS ambapo wanaamini watafanikisha mpango wa kuzipata point tatu na mabao matatu dhidi ya Kagera Sugar.