Faisary Ahmed – Kagera.

Wadau wa maendeleo Mkoani Kagera, wameandaa tamasha la maonesho ya biashara, kilimo, uwekezaji na utalii ya Afrika Mashariki, linalohusisha wafanyabiashara na wadau wa maendeleo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuukomboa mkoa huo kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa SPACT Company Limited ambao ni waandaaji wa maonesho hayo, Tumain Jasson amesema lengo la maonesho hayo ni kuufungua mkoa wa Kagera kiuchumi.

Amesema, “tunalenga kuufungua mkoa wa Kagera kiuchumi kwa maana kwamba wageni wote watakaoingia hapa watafikia kwenye hoteli zetu, watatumia vyombo vya usafiri na fedha za kigeni zitaongezeka kwahiyo serikali itapata mapato.”

Miongoni mwa washiriki wa maonesho hayo Frola Lauo kutoka Mwanza na Abrose Basizi wamesema kuwa maonesho hayo yatawasaidia kubadilishana uzoefu wa kibiashara na itawawezesha kupanua masoko ya bidhaa zao.

Kwa upande wake, mdau wa utalii Kagera na Mkurugenzi wa Kiroyera Tour, Mery Kalikawe amesema “kufikia mwaka 2025 lengo la taifa ni kufikisha watalii milioni 5 lakini bado tupo kwenye milioni 1.5, kupitia tamasha hili mkoa wetu utawavutia watalii wengi na itasaidia kufikia malengo hayo.”

Maonesho hayo, yaliyofunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa katika uwanja wa CCM Bukoba, yana kauli mbiu isemayo “Wekeza Mkoa Wa Kagera kwa maendeleo yako na Maendeleo ya Taifa” yakiwa na lengo la kuwakaribisha wadau mbalimbali, kuwekeza Mkoani Kagera.

Manula ashurutisha usajili mpya Simba SC
Msifumbie macho ukatili, ngono vyuoni - Mashine