Mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere amefunguka kwa mara ya kwanza kilichomuondoa Simba SC, baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio makubwa tangu msimu wa 2018/19 akitokea Gor Mahia ya Kenya.
Kagere aliondoka Simba SC mwanzoni mwa msimu huu, kufuatia mkataba wake kuvunjwa kwa makubaliano maalum na Uongozi wa klabu hiyo, na kisha alitimkia Singida Big Stars inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 36, amesema maamuzi ya aliyekua Kocha Mkuu Simba SC Zoran Maki, ndio yalimuondoka klabuni hapo kutokana na mapendekezo aliyowasilisha kwa viongozi.
Amesema Kocha huyo kutoka nchini Serbia alipendekeza kuwa na Washambuliaji wawili kwenye kikosi chake, na yeye kama mtu mzima alijiongeza na kuona hakuna nafasi tena Simba SC, hivyo ilikua rahisi kwake kuondoka, licha ya kuitwa kwenye meza ya makubaliano.
“Zoran alisema anataka washambuliaji wawili, viungo wawili na beki, nikajiuliza inawezekana vipi timu kuwa na washambuliaji wanne wa kigeni [Phiri, Mugalu, Kagere, Dejan] kichwani mwangu nikajiongeza ni dalili wananiambia tafuta timu nyingine hutakiwi,” amesema Kagere
Kagere alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kilichotwaa ubingwa wa Tanzania Bara mfululizo, huku akitoa mchango mkubwa kuifikisha klabu hiyo mara mbili hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na mara moja Kombe la Shirikisho Afrika.