Mshambuliaji wa Kimataifa wa Kenya Francis Nyambura Kahata amesema katika michezo inayofuata ya Ligi Kuu (VPL) na Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) moto wa kikosi Simba SC utakuwa zaidi ya ule wa mara ya kwanza kabla ya ligi kusimama.
Kahata ametoa kauli hiyo akiwa mazoezini Mo Simba Arena ambapo anaendelea kujiandaa katika Program maalum aliyopewa na kocha Sven, kufuatia kuchelewa kujiunga na wenzake, walipoanza maandalizi majuma mawili yaliyopita.
Kiungo huyo amesema maandaliazi anayoyaona kikosini kwa sasa ni makubwa, na anaamini moto wake utakua wa kuotea mbali katika michezo ya Ligi Kuu na Kombe La Shirikisho, ambapo wamedhamiria kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.
“Nafikiria tulikuwa miezi miwili karibia nyumbani na ukiangalia katika michezo miwili ambayo tumecheza wachezaji bado wanajituma sana, nafikiria moto ambao tulikuwa nao kabla ya Corona tutazidisha mara mbili yake pindi ligi itakapòanza june 14.” Amesema kiungo huyo.
Simba SC wataendelea na michezo ya Ligi Kuu mwishoni mwa juma hili kwa kuikabili Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa Dar es salam, huku wakipangiwa kukutana na Azam FC kwenye mchezo wa Robo Fainali wa Kombe La Shirikisho (ASFC), mwishoni mwa mwezi huu.
Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.