Viongozi Chama cha Msingi cha Ushirika cha zao la Kahawa Isansa, AMCOS wameamriwa kukamatwa na Jeshi la Polisi baada wakulima kulalamika kutolipwa fedha zao licha ya zao lao la Kahawa kuuzwa.
Agizo la kukamatwa kwa Viongozi hao limetolewa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akiendelea na ziara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, baada ya msafara wake kusimamishwa na wakulima wa kijiji cha Isansa wilayani Mbozi ambao walimueleza changamoto hiyo.
Awali, Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole alimuweleza Waziri Bashe kuwa AMCOS hiyo imekuwa ni mateso kwa wakulima kwa kushindwa kuwalipa fedha zao kwa wakati hivyo kumuomba awasaidie.
Mara baada ya kauli hiyo, ndipo Waziri Bashe alihoji kwa Katibu wa chama hicho cha ushirika, Sued Mgalla kuhusu Kahawa hiyo ambapo alisema imeuzwa na fedha zipo benki na hawajawalipa kwasababu bado walikuwa wanafanya mahesabu na ukaguzi wa madeni ya wakulima.
Kufuatia hatua hiyo, Bashe aliagiza Polisi wamkamate kiongozi huyo pamoja na wenzake, ili waweze kwenda kutoa fedha za wakulima walizodai zipo benki na kuongeza kuwa vitendo kama hivyo vimekuwa vikisababisha wakulima kuchukia ushiriki kwa makosa ya watu wachache wenye nia ovu.
Alisema, “Naomba hawa viongozi wasitoke ndani mpaka fedha za wakulima hawa zilipwe, na watafutwe viongozi wote wa ushirika, aiwezekani mkulima akope kwenye chama cha ushirika mifuko miwili ya mbolea auze kahawa yenye thamani Sh1.4 milioni halafu hela yake asipewe.”