Mtumishi wa Umma atakayeshindwa kuwasilisha cheti cha elimu na taaluma au “Index number” ya mtihani ili zihakikiwe na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), itakapofika tarehe 1 Machi, 2017atakua kajiondoa kazini mwenyewe.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah J. Kairuki alipokuwa akifungua mkutano wa watendaji Wakuu wa Wakala za serikali jijini Dar es saalm.
“Watendaji Wakuu ninawaomba msimamie uhakiki wa vyeti ili watumishi wenu wafanye kazi kwa sifa stahiki” amesema Kairuki.
Waziri Kairuki amewataka Watendaji Wakuu kuweka mikakati ya kuepuka watumishi hewa na kusimamia kwa dhati kwasababu jambo hilo limeumiza na kupoteza rasilimali fedha nyingi za Serikali.
Amesema anatambua kuna Wakala zenye upungufu wa Watumishi hivyo zinaingia gharama kubwa za kuajiri wafanyakazi wa mikataba, hata hivyo ameelekeza kila Mtendaji Mkuu ajiridhishe kwa kuandaa taarifa ya mahitaji halisi ya Watumishi.
Aidha, pamoja na hilo ameelekeza Wakala zenye Watumishi wa mikataba zifanye tathmini na kuhakiki kama kweli watumishi hao wanahitajika kwa kuwa eneo hilo ni moja ya maeneo yenye ajira za mashaka kwa baadhi ya Taasisi.
Hata hivyo, ameongeza kuwa malalamiko kuhusu suala la maadili na uwajibikaji yanayozigusa Wakala za Serikali. ikiwa ni pamoja na Watumishi hewa, taarifa chafu za Watumishi, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za Umma, kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa mifumo ya utendaji kazi na wakati mwingine kutotekeleza majukumu ya msingi ya wakala.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi Dkt. Laurean Ndumbaro amezitaka Wakala za Serikali kuimarisha eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuimarisha utendaji kazi na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania.