Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia ulinzi na kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite na watakaokwenda kinyume na matakwa ya Sheria, kiama chao kinakuja.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani Manyara alipotembelea migodi mbalimbali ya madini ya Tanzanite ndani ya ukuta wa Mirerani.

Amesema kuwa ziara hiyo imelenga kuangalia suala zima la ulinzi katika ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite, shughuli za uchimbaji madini mengine zinavyofanyika na kuangalia namna uzalishaji wa madini ya Tanzanite  unavyoendelea katika migodi husika.

Aidha, ameongeza kuwa ziara hiyo pia imelenga kuangalia namna Sheria ya Madini inavyotekelezwa, masuala ya Mikataba ya watumishi katika migodi na namna migodi husika inavyolipa kodi mbalimbali za Serikali yakiwemo masuala ya usalama sehemu za kazi na  wafanyakazi kwa ujumla.

“Utoroshaji madini hausaidii, fedha ni za haraka lakini zinawaadhibu Watanzania walio wengi kwa kuwa, fedha hizo hizo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo. hivyo kila mtanzania awe mlizi wa mwenzake,” amesema Kairuki.

Hata hivyo, Kairuki ameongeza kuwa serikali inatambua mchango wa wachimbaji wadogo katika kuchangia pato la taifa kupitia shughuli za uchimbaji, hivyo akawaasa wachimbaji nchini kufuata Sheria, kanuni na taratibu ili kufanya shughuli halali ikiwemo kulipa kodi stahiki.

 

Hospitali za serikali zaonywa kuwalipisha wajawazito, wazee na watoto
Alisson Becker kuvaa gwanda dhidi ya SSC Napoli