Wapinzani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Robo Fainali Kaizer Chiefs, wapo jijini Dar es salaam, tayari kwa mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa kesho Jumamosi (Mei 22) Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia mishale ya saa kumi jioni.

Kaizer waliwasili jijini Dar es salaam jana jioni, wakitokea moja kwa moja Afrika Kusini, na leo wanatarajia kufanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kabla ya kuanza safari, Uongozi wa klabu hiyo ambayo ilibugiza Simba SC mabao manne kwa sifuri kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Jumamosi (Mei 15) mjini Johannesburg Afrika kusini, uwanja wa FNB (Soccer City) ulitoa taarifa za kuwafanyia vipimo vya ugonjwa wa Corona (Covid 19) wachezaji wote, na majibu yalionesha hawana maambukizi.

“Kikosi kabala ya kusafiri pia kilifanya vipimo vya Covid-19 kama inavyotakiwa na sheria kabla ya kusafiri nje ya nchi.”

“Tulipokea majibu safi ya vipimo vyetu vya Corona kwa mara ya pili chini ya siku saba.”

“Kama inavyotakiwa na sheria za CAF, timu yetu inatarajiwa kufanya vipomo kwa mara nyingine Dar es Salaam kabla ya mchezo wetu dhidi ya Simba na tuna hakika kwamba tutapata usawa na uwazi kama ilivyokuwa kwenye  safari zetu zote kwenye nchi nyingine, kama Angola, Burkina Faso, Guinea na Cameroon.”

“Tumepokea ripoti za wasiwasi baadhi ya manung’uniko juu ya majibu ya vipimo kuchezewa lakini tunaamini kuwa hatutapata chochote cha aina hiyo kutoka kwa mamlaka za Tanzania.”

“Simba kama timu zingine ambazo zimetutembelea kwa mchezo wetu wa nyumbani walipokelewa katika mazingira safi na ukarimu wa hali ya juu na tunatumai Watanzania watarudisha neema.”

“Tunaamini Mpira wa miguu ni mchezo unaochezwa uwanjani na matokeo yanapaswa kuamuliwa uwanjani.”

“Tufanye kazi pamoja kama Waafrika na tuonyeshe ulimwengu kuwa tuna uwezo wa kuungana.”

Lamine Moro kujitetea Young Africans
Israel na Palestina zasitisha mapigano