Gwiji wa klabu ya AC Milan, Ricardo Izecson dos Santos Leite (Kaka) amesema ana mpango wa kurejea klabuni hapo kwa ajili ya kujifunza masuala ya utawala wa soka, kama ilivyo kwa magwiji wenzake Leonardo na Paolo Maldini ambao kwa sasa ni viongozi.
Kaka mwenye umri wa miaka 36, amesema mpango huo anatarajia kuukamilisha mara baada ya kufikia hatua ya kustaafu soka mwaka 2017, akiwa na klabu ya Orlando City inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Marekani (MLS).
Amesema utawala wa soka ni suala muhimu katika maisha yake, na alijipangia kufanya hivyo tangu akiwa mchezaji wa AC Milan kuanzia mwaka 2013–2014, lakini shughuli za kucheza soka zilimzuia kutimiza ndoto hiyo kwa wakati huo.
Hata hivyo amedai kuwa rafiki zake Leonardo na Paolo Maldini ambao walicheza kwa pamoja AC Milan, wamekua wakimshawishi kurejea Italia na kujifunza mambo kadhaa ya utawala wa soka, na ameona kuna ulazima wa kufanya hivyo kutokana na kuhitaji kuutumikia mchezo huo ambao unamuendeshea maisha yake ya kila siku.
“Nilitamani tangu zamani kuwa kiongozi wa soka, lakini nilishindwa kufanya hivyo kwa sababu nisingeweza kuwa mchezaji, na hapo hapo kiongozi,” alisema.
“Sina mahala pengine pa kwenda kujifunza masuala ya utawala wa soka zaidi ya AC Milan kwa sasa, nilipapenda na ninaendelea kupapenda kutokanana mazingira yake kunivutia tangu nikiwa mchezaji hadi sasa nimeshastaafu,” alifafanua.
“Sihitaji kuwa kocha wa soka, ninahitaji kuwa kiongozi wa juu, kama ilivyo kwa rafiki zangu Leonardo na Paolo Maldini ambao kwa sasa ni watendaji wakubwa katika klabu ya AC Milan.”
Alieleza kuwa anaamni watamfundisha mambo mengi, kwa sababu ni watu ambao wamekua wakimshawishi kurudi Italia na kujionea namna wanavyoendesha klabu ya AC Milan tangu alipokabidhiwa majukumu ya kuwa watendaji.