Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe amefunguka mbele ya vyombo vya habari leo hii mara baada ya kuachiwa na watu wa Uhamiaji waliokuwa wanamfanyia mahojiano katika ofisi zilizopo kurasini, jijini Dar es salaam.
Ambapo amesema kuwa mahojiano hayo yaligusa moja kwa moja kuhusu uraia wake ambapo amehojiwa maswali mengi kuthibitisha kama ukweli askofu huyo ni raia wa Tanzania, mbali na mahojiano hayo amesema kuwa idara hiyo imefanikiwa kuchukua hati zake nne anazotumia kusafiria, kwa ajili ya kuthibitisha baadhi ya taarifa zinazopatikana katika hati hizo.
Aidha amesema kuwa idara hiyo imejiridhisha kuwa yeye ni raia wa Tanzania.
Katika mazungumzo yake amelinganisha tukio hilo na maandiko katika biblia amesema kuwa Methali 28:1 Biblia inasema,
”Muovu anakimbia hata kama hajafuatwa na mtu, lakini mwenye haki ni jasiri kama simba”, hivyo amesema yeye ni jasiri kwani hana hatia yeyote.
Amesema ”Mimi sina uovu wowote mimi ni raia wa nchi hii, kwahiyo nimetoa maelezo yote ya kina kwamba mimi ni raia wa hapa” amesema Kakobe.
Lakini pia amegusia kuwa utafiti juu ya uraia wake umeanza kufuatiliwa muda mrefu ambapo kuna watu wamekuwa wakitumwa kijijini kwake kuthibitisha uraia wake na kukuta hana hatia yeyote.
Aidha ameongezea kuwa bado hajafahamu sababu za idara hiyo kufuatilia uraia wake.