Baada ya kuambulia patupu katika mashindano ya Ngao ya Jamii, Mlinda Lango wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya, amesema yuko tayari kwa mikikimikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inaanza rasmi leo Jumanne (Agosti 15).
Kakolanya amesema timu yake imefanya maandalizi mazuri na anaamini makosa yaliyojitokeza katika michuano hiyo atayafanyia kazi na hatimaye kuwa na msimu mzuri wa mwaka 2023/2024.
Mlinda Lango huyo amesema ana uhakika na kiwango chake kitaongezeka kutokana na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara baada ya kujiunga na timu hiyo mpya akitokea Simba SC.
“Nina imani kubwa na timu yangu kufanya vizuri, kila mmoja kwenye kikosi anataka kusaidia timu kufanya vizuri, tumemaliza michuano hii, kwa sasa nguvu zetu zinahamia katika mashindano ya kimataifa, tunaenda kupambana,” amesema Kakolanya.
Ameongeza anatarajia msimu mpya utakuwa mgumu kutokana na uimara wa timu zote ambazo zimejiimarisha kwa ajili ya kuonyesha ushindani.
“Mimi nadhani msimu ujao ligi itakuwa ngumu zaidi, timu zimesajili kwa kadiri ya nguvu zao, ligi itakuwa ngumu na ninamaanisha ushindani utaongezeka sana,” Kakolanya amesema