Mlinda Lango chaguo la pili katika kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Beno Kakolanya, huenda akaanza langoni leo Ijumaa (Machi 04), katika mchezo wa Mzunguuko wa 16 dhidi ya Biashara United Mara.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo, Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam kuanzia saa moja usiku huku ikiwa na matumaini makubwa ya kupata alama tatu kwa wageni wao kutoka mkoani Mara.

Mkuu wa Benchi la Ufundi la Simba SC Pablo Franco Martin, amesema Mlinda Lango chaguo la kwanza kwenye kikosi chake Aishi Manula, hatakuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Biashara United Mara, kufuatia matatizo ya kifamilia yanayomkabili katika kipindi hiki.

Amesema kutokupo kwa Malinda Lango huyo, kutatoa nafasi kwa wasaidizi wake ambao ni Beno Kakolanya na Ally Salim kuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kitakachokuwa na jukumi la kusaka alama tatu nyumbani.

Hata hivyo asilimia kubwa ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza ipo kwa Mlinda Lango Beno Kakolanya ambaye ni chaguo la pili na Ally Salim siku zote amekua chaguo la tatu.

Simba SC itakua na kumbukumbu ya kuambulia sare ya kutokufungana dhidi ya Biashara United Mara, katika mchezo wa Mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu, uliopigwa Uwanja wa Karume mjini Musoma Mkoani Mara.

Biashara United Mara wao watakua na jukumu la kutaka kuendeleza furaha ya ushindi, baada ya kuibanjua Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa Mzunguuko wa 15 uliopigwa jijini Mwanza juma lililopita.

Young Africans yaifuata Geita Gold Mwanza
Mwaka mmoja wa Rais Samia: Vifo vingi vimeepukika katika sekta ya afya