Mlinda Lango aliyeondoka Simba SC Beno Kakolanya amesema, kuna faida kubwa katika timu hiyo kuwa na Mhambuliaji kutoka Zambia Moses Phiri, kutokana na ubora alionao.
Kakolanya amesema endapo Phiri asingepata majeraha anaamini angekuwa mfungaji bora wa msimu uliopita ambao Fiston Mayele na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ walimaliza na mabao 17 kila mmoja.
Amesema anaamini Phiri ni mshambuliaji mahiri kuliko wote waliopo Simba SC kutokana na ubora wake wa kutumia miguu miwili ambayo mara nyingi inakuwa inawachanganya makipa kutojua anapiga na upi wakati gani.
“Phiri ni Mshambuliaji hatari. Wakati tumeweka kambi Misri nilimsoma mazoezini. Kwanza uamuzi wake wa haraka unapompigia mahesabu ya kumzuia kwa namna hii tayari anakuwa ameishafanya uamuzi wa kuupiga mpira kwa jinsi ambavyo hujatarajia. Hivyo anapaswa kuchungwa muda wote.
“Ana uwezo mkubwa wa kusoma mabeki na kipa, anaweza akawa na mpira ukampuuza, lakini atakachofanya unabakia kushangaa, Jamaa asingeumia nina uhakika asilimia 100 angechukua kiatu cha ufungaji.”
“Anachokifanya mazoezini anakiingiza uwanjani anafanya zaidi na anatoa uhakika wa kupata mabao.” amesema Kakokalanya.
Kipa huyo amesema anaamini Phiri msimu ujao akipata nafasi ya kucheza, basi Simba SC inaweza kuvuna mabao mengi kupitia Mshambuliaji huyo, ambaye alisisitiza ni hatari akiwa na mpira.
Ukiachana na stori za Phiri, Kakolanya amesema muda mfupi ujao kila mtu atafahamu anakwenda timu gani: “Siwezi kukosa timu ya kucheza. Siyo muda mrefu itajulikana nitacheza wapi.”
Licha ya kuficha jina la timu tayari imeshafahamika Kakolanya anakwenda kuitumikia Singida Fountain Gate FC.