Mlinda Lango wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya amesema licha ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future ya Misri utapigwa ugenini, lakini anaiona nafasi ya timu yao kutinga makundi ya michuano hiyo.
Timu hizo zitakutana Oktoba Mosi katika Uwanja wa Al-Salaam, Cairo, Misri, huku Singida ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 ilioupata juma lililopita Dar.
Akizungumzia mchezo wa ugenini, Kakolanya amesema Simba SC na Young Africans zimejiweka pazuri kutinga makundi Ligi ya Mabingwa, lakini wao ni ngumu kwa kuwa walianzia nyumbani na ushindi mwembamba.
Hata hivyo, Mlinda Lango huyo wa zamani wa Young Africans na Simba SC amesema ushindi waliopata nyumbani unawapa nguvu ya kutinga makundi na kwamba kila mchezaji atajitolea kuhakikisha anapata matokeo mazuri.