Rapa Kala Jeremiah amekumbuka machungu ya kutafuta nafasi ya kufanikiwa kwenye kiwanda cha muziki ambapo alijikuta akilazimishwa kuimba kama mchekeshaji Kingwendu.
Kala wa Mwanza amedai kuwa baada ya kutoka Mwanza na kuingia jijini Dar es Salaam akijaribu kutafuta nafasi, alikutana na mwandishi wa gazeti la Nipashe ambaye alisikia historia yake ya muziki na kuipenda lakini mbali na kumuandika kwenye gazeti la Nipashe aliampa msaada kwa kumkutanisha na rafiki yake ambaye alikuwa mtayarishaji wa muziki.
Akifunguka kupitia The Playlist ya Times FM, Kala alidai kuwa baada ya kukaa kwa muda akimsubiri mtayarishaji amalize kazi yake aliyomkuta akiendelea nayo, mtayarishaji huyo alimtaka aimbe kidogo ili aone kipaji chake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Kala, baada ya kuchana kwa moyo akichagua kilicho bora zaidi kutoka kwenye maktaba yake, mtayarishaji huyo alimtaka aachane na mtindo aliokuwa anaimba badala yake aimbe kama Kingwendu aliyekuwa anavuma na wimbo wa ‘Mapepe’.
“Alivyomaliza kazi yule jamaa aliniita akanisikiliza, ‘nikachanaaa’ mwanzo mwisho, mistari mizuri tu. [Baadaye] akabonyeza kitufe likaanza kulia ‘Mapepe’ la Kingwendu, ndilo limetoka lina siku mbili au tatu,” alifunguka.
“Akaniambia, ‘kama unataka mchongo na mimi, piga mangoma kama haya’,” aliongeza.
Rapa huyo wa Dear God anasema baada ya kusikia kauli ya mtayarishaji huyo, alijisikia vibaya na kumpa ukweli na msimamo wake kuwa hawezi kukubaliana na masharti yake ingawa alikuwa ana kiu ya kutoka kimuziki.
Anasema msimamo wake ulitokana na kujitambua kuwa anahitaji kubaki kwenye msingi wa maisha yake bila kufuata kiu ya kutaka kupata umaarufu mapema.
Mfano huo ulikuwa ni moja kati ya ushauri aliokuwa anautoa Kala kwa wasanii wachanga wanaotafuta mafanikio kwenye muziki kwamba wanatakiwa kujiwekea msingi na misimamo ya kile wanachoamini wanataka kufanya bila kufuata upepo.
Hivi karibuni, Kala aliachia audio na video ya wimbo wake mpya ‘Natabiri’ akimshirikisha Walter Chilambo.