Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemanii amepiga marufuku uagizwaji wa nguzo za umeme, Transfoma na nyaya za umeme nje ya nchi badala yake Tanesco waongee na wahusika ili wajenge viwanda vya kuzalisha vifaa hivyo hapa nchini.
Kalemani ametoa agizo hilo mapema hii leo kwa Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO kufuatia gharama kubwa ya vifaa hivyo vikiagizwa nje ya nchi tofauti na vitakapozalishwa hapa nchini.
“TANESCO nawaagiza kuacha mara moja kuagiza vifaa hivyo nje ya nchi, kwani ni gharama kubwa sana inayotumika, fanyeni mpango wa kufanya mazungumzo na wahusika ili wawekezaji waje kufungua viwanda hapa nchini vya kuzalisha bidhaa hizo,”amesema Dkt. Kalemani.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kama vifaa hivyo vitazalishwa hapa nchini basi gharama ya manunuzi itakuwa chini hivyo vitapatikana kiurahisi na kuzalisha ajira kwa Watanzania wengi.