Benchi la ufundi la Azam FC limetangaza kupambana kusaka ushindi katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara dhidi ya Wekundu wa Msimbazi Simba SC.
Azam FC itacheza dhidi ya Simba SC katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kesho Jumapili (Mei 07).
Kaimu Kocha Mkuu Azam FC Kally Ongala, alisema wachezaji wao wana morali kubwa kuelekea katika mchezo huo na wanaamini ndoto zao za kubeba taji hilo msimu huu litatimia.
Kally amesema kila mchezaji ameahidi kupambana kuhakikisha wanapata ushindi mapema huku wakiwaheshimu Simba SC ambayo bado ina joto la mashindano ya kimataifa.
“Itakuwa ni mechi ya kulipa kisasi, hatutakubali tutolewe kirahisi na Simba, lengo letu ni kupambana kuhakikisha tunaingia hatua ya fainali,” amesema Ongala.
Aliongeza wameimarisha safu yao ya ushambuliaji ili wapate matokeo mazuri na wanawataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwaunga mkono kwa sababu wamejipanga kuwapa furaha.
Tayari vikosi vya Simba SC na Azam FC vimewashawasili mjini Mtwara kwa ajili ya mchezo huo, ambao umepangwa kuanza kuunguruma majira ya saa tisa alasiri.
Timu hizo zinakutana huku Azam FC ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza bao 1-0 katika hatua ya Nusu Fainali ya michuano hii msimu wa 2020/21, lililofungwa na mchezaji wake wa zamani, Luis Miquissone baada ya mabeki kuzembea.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Majimaji mjini Songea Mkoani Ruvuma, Miquissone alifunga bao hilo dakika ya 89 baada ya mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Bernard Morrison anayeicheza Young Africans kwa sasa kuanzisha kwa haraka mpira wa kutenga ‘Free-Kick’.