Kocha wa Azam FC, Kally Ongala amefichua sababu zilizopelekea kikosi chake kushindwa kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ mbele ya Young Africans.
Azam FC ilishindwa kufikia malengo ya kumaliza msimu ikiwa na kitu mkononi, kwa kuambulia patupu, baada ya kukubali kupoteza kwa 1-0, katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga jana Jumatatu (Juni 12).
Kally amesema mchezo huo wa Fainali ulikuwa mzuri na wachezaji wake walionesha uwezo wa kupambana, japo bahati ya kuibuka na ushindi haikuwa kwao.
Amesema kwa asilimia kubwa wachezaji wake walitengeneza nafasi nyingi katika lango la Young Africans hasa katika kipindi cha pili, lakini walishindwa kuzitumia.
Hata hivyo Kocha huyo amesema Azam FC imejifunza mengi katika msimu wa 2022/23, hivyo anatarajia makubwa kutoka kwenye timu hiyo kwa msimu ujao 2023/24 ambao umeanza kutabiriwa huenda ukawa na ushindani wa hali ya juu.
“Kwa hakika wachezaji wangu walionesha uwezo wa kupambana dhidi ya Young Afrcans, walionesha kuwa tayari kushinda mchezo lakini haikuwa hivyo, kipindi cha pili walitengeneza nafasi nyingi sana lakini walishindwa kuzitumia.”
“Naiona Azam FC nzuri msimu ujao, hatukufanikiwa kutwaa taji lakini nimeona kitu ambacho tunaweza kukianza tena msimu ujao, bila shaka tuna mwendelezo mzuri,” amesema Ongala
Licha ya kupoteza mchezo huo wa Fainali, Azam FC bado ina nafasi ya kushiriki Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ msimu ujao, kufuatia Tanzania kuwa na nafasi nne kikanuni.
Kwa kanuni hiyo Young Africans na Simba SC zitaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Azam FC na Singida Big Stars zikitarajia kushiriki Kombe la Shirikisho Barani humo.