Kamanda Mwandamizi wa Kundi la Kigaidi la Al-Shabaab, Bashir Mohamed Qorgab ameuawa katika shambulizi la anga lililofanywa na Jeshi la Marekani nchini Somalia.

Shirika la Habari la Somalia limeripoti kuwa kamanda huyo aliuawa Februari 22, 2020 lakini taarifa hizo hazikutangazwa kwa sababu za kiintelijensia. Familia ya Qorgab imethibitisha kifo chake.

Marekani ilitangaza zawadi ya $5 milioni kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa za alipo kamanda huyo tangu mwaka 2008.

BBC imeripoti kuwa Marekani ambayo inafanya mashambulizi mengi ya anga nchini Somalia haijazungumzia taarifa ya kifo cha kamanda huyo.

Bashir Mohamed Qorgab alikuwa kiongozi wa mstari wa mbele wa mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi na mashambulizi mengine yaliyokuwa yanafanywa na kundi hilo nchini Kenya.

Kundi la Al-Shabaab ni mshirika wa Kundi la kigaidi la Al-Qaeda na linadhibiti sehemu kubwa ya kusini na kati mwa Somalia.

Vandenbroek aomba radhi, Eymael ajivunia kuvunja mwiko
Iran: Maambukizi ya Corona yaongezeka