Jeshi la polisi Mkoani Songwe limezungumzia tukio la askari watatu wa usalama barabarani kumpa kibano dereva wa fuso katika mji wa Tunduma mkoani humo.
Ufafanuzi wa jeshi hilo umekuja kufuatia kusambaa kwa kipande cha video kinachoonesha tukio hilo, ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alieleza kuwa amemtumia Kamanda wa Polisi wa Songwe ili afanye ufuatiliaji.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Yusufu Sarungi ameeleza kuwa askari hao walikuwa wakitekeleza jukumu lao la kumdhibiti dereva huyo aliyetumia lugha chafu na kukaidi maelekezo halali ya askari hao.
Kaimu Kamanda Sarungi ameeleza kuwa Januari 12 mwaka huu majira ya saa mbili asubuhi, askari wao walikuwa kwenye zoezi la ukaguzi wa magari wakishirikiana na maafisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), walipokutana na dereva huyo aliyeonesha ujeuri.
Alisema dereva huyo anayefahamika kwa jina la Mawazo Jairoz, mkaazi wa Mbeya aliyekuwa akiendesha gari aina ya Mitsubishi- Fuso yenye namba za usajili T842 AAC, alisimamishwa awali lakini alitoa lugha za matusi dhidi ya askari na maafisa wa Sumatra na kisha kuondoa gari akipitia barabara ya vumbi.
Aidha, kwa mujibu wa Sarungi, askari hao walimfuatilia na kumkamata katika eneo la Makambini wilayani Momba, ambapo walijaribu kumdhibiti lakini baadhi ya wananchi waliingilia na kuachanisha.
Alisema baada ya kupata upenyo, Jairoz alikimbilia kwenye gari na kuchukua panga akiwatishia askari hao, ndipo alipofanikiwa kuondoa gari katika eneo hilo, lakini alikamatwa tena katika mji wa Vwawa.