Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imelipongeza Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kuendesha Mfuko wa Taifa Kuendeleza Wajasiliamali Wananchi (NEDF) kwa mafanikio na kulitaka Shirika hilo kuongeza ubunifu katika kutafuta njia za kutunisha mtaji wa Mfuko huo ili kuwawezesha wananchi wengi mijini na vijijini kuanzisha viwanda vidogo vidogo.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Erick Shigongo (Mb) wakati  wa utoaji wa Taarifa  ya utekelezaji wa Mfuko (NEDF)  kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira, jijini Dodoma.

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali  yanayolenga kuboresha Mfuko wa NEDF katika kutafuta njia za kuongeza  fedha za mtaji wa Mfuko, utoaji wa mikopo mijini na vijijini kwa kuzingatia makundi maalumu, muundo wa uendeshaji, viwango vya mikopo, vigezo vya kupata mikopo, riba ya mikopo hiyo na ufadhili wa vikundi vya wajasiliamali.

Naye, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.)  aliihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa  ili kuhakikisha SIDO inawezeshwa na inaongezewa mtaji katika Mfuko wa NEDF ili kuongeza kasi ya uanzishaji na ukuzaji wa viwanda vidogo nchini ambavyo vitaongeza ajira na kukuza biashara na uchumi wa nchi.

Naye, Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe alisema ni muhimu kuiwezesha SIDO kuongeza mtaji katika Mfuko huo wa NEDF kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha pamoja na  kishirikiana na taasisi za umma ili Mfuko huo uweze kusaidia wananchi wanaohitaji mitaji ya kuanzisha viwanda vidogo vya kuzalisha bidhaa mbalimbali.  

Awali, akitoa utoaji wa Taarifa  ya utekelezaji wa Mfuko (NEDF), Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji alieleza kuwa Mfuko huo unaopatikana mikoa yote umeweza kudumu tangu mwaka 1994 ulipoanzisha na umepokea jumla ya Shilingi 6,648,886,000 katika kipindi cha 1994/1995 hadi 2020/2021 kama mtaji na kuukuza hadi Shilingi 9,765,670,054.

Afisa ustawi wa jamii anyongwa
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 6, 2022