Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula amesema Kamati hiyo imeridhishwa na kasi ya Ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere( JNHPP) na kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa mradi huo.

Kitandula amesema hayo wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati hiyo inayolenga kukagua maendeleo ya Miradi mbalimbali mkoani Pwani, katika sekta ya Nishati inayotekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.

Amesema kuwa baada ya kuona hali halisi ya utekelezaji wa mradi huo kwa sasa Kamati hiyo inatembea kifua mbele ikijivunia kazi kubwa iliyofanyika na inayoendelea kufanyika kukamilisha mradi huo kwa wakati.

“Kwa mara ya kwanza wakati wazo la kutekelezwa kwa mradi huu lilivyotolewa, Kamati tulifurahia sana kuona ndoto ya Baba wa Taifa inaenda kutimia na kuweka historia mpya ya nchi yetu, na tuliadidi kuwaeleza watanzania mpaka watuelewe juu ya mradi huo mkubwa unaogharimu fedha nyingi, watanzania wajivunie kuwa na mradi huu mkubwa utaokamilika ndani ya muda uliopangwa na utakuwa na manufaa makubwa sana ndani na nje ya nchi,” amesema Kitandula.

Aidha, amesema kuwa, wamefurahishwa na kitendo cha Serikali kulipa kwa wakati fedha za mkandarasi anayetekeleza mradi huo kwa kila hatua ya ujenzi wa mradi inapofikia.

Sambamba na hilo ameipongeza Serikali ya awamu ya Tano, kwa kuthubutu na kutekeleza mradi huo, ulioasisiwa na Baba wa Taifa zaidi ya miaka 40 iliyopita, na kuupa kipaumbele kwa kutenga fedha za kutekeleza mradi husika

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani ameieleza Kamati hiyo kuwa imekuwa ni chachu ya kutekeleza mradi huo baada ya kuridhia na kupitisha bajeti ya kutekeleza mradi huo pamoja na kuwa bega kwa bega na Wizara ya Nishati kuhakikisha mradi huo unatekelezwa.

Mradi wa JNHPP utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2115 na kuifanya Tanzania kuwa na Jumla ya Megawati 4848, huku mahitaji halisi kwa nchi zima yakitarajiwa kuwa ni Megawati 2700.

Kenya yapiga marufuku mikutano ya kisiasa
Taifa Stars kuifuata ‘Harambee Stars’ kesho