Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Ramadhani, Halmashauri ya mji wa Njombe mkoani Njombe imesema haitaweza kusitisha zoezi la wazazi kuchangia fedha kiasi cha shilingi elfu thelathini kwa ajili ya madawati kwa kuwa hakuna mzazi yeyote katika kata hiyo anayependa mtoto wake kukaa chini.
Siku chache zilizopita Mkuu wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri alilazimika kusitisha zoezi la kuchangia kiasi hicho cha fedha na kuagiza kushushwa vyeo afisa elimu wa kata ya Ramadhani Estar Mjululu, na Huruma Mgeyekwa pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari Maheve, Valeno Kitalika kwa makosa ya kuandika mchango wa kiasi hicho cha fedha katika fomu za kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza
Diwani wa Kata ya Ramadhani, George Sanga amesema kuwa wananchi wa kata hiyo wameipokea taarifa ya mkuu wa wilaya ya kuzuia wazazi kuchangia dawati kwa masikitiko makubwa licha ya kazi hiyo kutakiwa kufanywa na serikali lakini wananchi walikubaliana ili kupunguza changamoto ya madawati katika shule yao.
“Zoezi hili limeleta mtafaruku kidogo kwa wananchi wa Ramadhani, sababu ya ujenzi haiwahusu wao ni wataalamu wanashauri kikao changu na tunaupokea ushauri lakini sio kwa sura ya kuwachanganya wananchi kwa kujitolea michango yao mifukoni, kazi hizi zipo wazi zinatakiwa kufanywa na serikali,”amesema Sanga
Aidha, baadhi ya wananchi wa kata hiyo akiwemo, Meshack Kawogo wakizungumza na Dar24 Media wamesema kuwa ni vyema kuendelea kuchangia madawati pamoja na serikali kuwasaidia kutokana na kuona upungufu wa madawati.
-
Wakorinto wakutana uso kwa uso na viongozi wa CCM Njombe
-
DC Msafiri acharuka, awaweka kikaangoni watendaji
-
Video: Mhandisi Kilaba aufagilia mfumo wa TTMS
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Diwani huyo amesema kuwa shule ya Sekondari Maheve iliyopo katika Kata yake, mpaka sasa ina upungufu wa viti 92 na meza 92 kwa jumla ya wanafunzi 684 huku kukiwa na uhaba wa vyumba viwili vya madarasa ambapo mpaka sasa wanaendelea na ujenzi wa madarasa matatu ambayo yanakaribia kukamilika.