Kamati ya Nidhamu iliyokutana Jumamosi Februari 10, 2018 pamoja na mambo mengine pia ilipitia shauri la mchezaji wa Kagera Sugar Juma Nyoso lililofikishwa kwenye kamati akituhumiwa kwa utovu wa nidhamu kwenye mechi namba 112 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Kagera Sugar dhidi ya Simba Sports Club iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Juma Nyoso alituhumiwa kumpiga shabiki baada ya kumalizika mchezo huo kinyume cha kanuni ya 36 ya ligi Kuu inayozungumzia uchezaji wa kiungwana pamoja na Ibara 50(1)(2) na (5) ya katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati ilipitia ripoti ya kamishna wa mechi ambayo imeeleza tukio hilo la Juma Nyoso kupishana na shabiki aliyekuwa amebeba vuvuzela na ndipo Nyoso aliposimama na kuanza kumpiga na kiatu na kutumia goti mpaka askari wa jeshi la Polisi walipoingilia kumuokoa na kumshikilia mchezaji huyo wakati shabiki akipatiwa huduma kwenye gari la huduma ya kwanza.
Juma Nyoso katika utetezi wake alikana malalamiko dhidi yake akidai kitendo alichofanya ni kukunjana na shabiki.
Kamati kupitia ripoti ya kamishna wa mchezo huo imemtia hatiani Juma Nyoso kupitia kanuni ya 36 ya kanuni ya Ligi kuu na Ibara ya 50(1)(2) na (5) ya katiba ya TFF.
Kamati pia ilipokea taarifa za nyuma za nidhamu za Juma Nyoso ambayo rekodi inaonesha aliwahi kufungiwa kwa makosa ya kinidhamu .
Kupitia kifungu cha 37(10)cha kanuni za ligi Kuu kamati imemtia hatiani Juma Nyoso na imemfungia kutocheza mechi Tano(5) na faini ya Shilingi milioni moja(1,000,000).