Kamati ya Taifa Stars chini ya Mwenyekiti, Faroukh Baghoza imekutana usiku huu katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo imekutana ikiwa ni kwa ajili ya kupanga mikakati pamoja na kuunda kamati ndogondogo.
Kamati hiyo pia ilitoa nafasi kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kutoa maoni yao kwa lengo la kuhamasisha na kuisaidia Taifa Stars kuitoa Algeria katika mchakato wa kuwania kucheza Kombe la Dunia, Novemba.
Stars inawania kucheza Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018 na sasa itakutana na Algeria ikiwa ni baada ya kuitoa Malawi.
Katika mkutano huo chini ya Baghoza na katibu, Teddy Mapunda, kamati hiyo iliwapa wadau wakiwemo waandishi wa habari kutoa maoni yao katika masuala kadhaa yakiwemo ya uhamasishaji kwa Watanzania.
Mengi yalizungumziwa na baada ya hapo, mapendekezo hayo yatapelekwa kwenye kamati ndogondogo ambazo zitagawanya majumu ili kuharakisha utendaji.
Lengo kuu la kamati hiyo ni kusaidia kufanikisha ushindi kwa kuviong’oa vigogo, Algeria ambao ndiyo timu bora Afrika kwa kipindi hiki.
Kamati ya Taifa Stars imepewa majukumu manne na rais wa TFF Jamal Malinzi ambayo ni
(i) Kuimarisha huduma kwa wachezaji,
(ii) Uhamasishaji na Masoko,
(iii) Kuhamasisha wachezaji,
(iv) Kuandaa na kusimamia mkakati wa Ushindi.
Kamati hii inaongozwa na Mwenyekiti Farough Baghouzah, Teddy Mapunda (Katibu), Wajumbe ni Juma Pinto, Michael Wambura, Iman Madega, Salum Abdallah na Isaac Chanji.