Hatimaye Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeamua uchaguzi uliokuwa na mgogoro wa klabu ya Lipuli FC ya Iringa, kufanyika Agosti 5 mwaka huu.
Uamuzi huo umefIkiwa kufuatia mkutano wa kamati hiyo wa Juni 10 na 11 mwaka huu ambao pamoja na mambo mengine, kamati ilijadili suala la uchaguzi wa klabu hiyo ambao awali ulipangwa kufanyika Mei 29 mwaka huu lakini ukagubikwa na malalamiko ya wanachama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, kamati hiyo iliamua kufuatilia taratibu mbalimbali, kanuni na sheria na kujirisha katika yote. Hivyo, imeamua kuwa mchakato wa uchaguzi huo utaanza upya kuanzia Juni 27, mwaka huu na uchaguzi utafanyika Agosti 5 ukisimamiwa na kamati hiyo kama ilivyopangwa awali.
TFF imeeleza kuwa uamuzi huo umezingatia malalamiko yaliyoletwa na wanachama ambao baadhi ya majina yaliondolewa kwenye daftari la usajili la wanachama. Hivyo, zoezi jipya la kuchukua na kurejesha fomu litaanza Juni 28, mwaka huu.