Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imepokea kesi ya kupinga uchaguzi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) uliopangwa kufanyika Jijini Tanga Agosti 07.
Taarifa iliyotolewa jioni hii imeeleza kuwa Mahakama hiyo imemtaka Rais wa TFF Wallace Karia, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi na Bodi ya Wadhamini ya Shirikisho hilo kufika Mahakamani hapo kujibu hoja za kwa nini uchaguzi wa TFF usisimamishwe.
Wito kwa viongozi hao unapaswa kuitikiwa kesho Ijumaa saa 3 asubuhi.
Hata hivyo hadi sasa hakuna taarifa za aliyefungua kesi ya kupinga Uchaguzi Mkuu wa TFF, licha ya kuwa aliyekuwa mgombea nafasi ya Urais Ally Saleh ‘Alberto’ kuwahi kutushia kwenda Mahakamani kwa lengo la kupata ufafanuzi wa baadhi ya kanuni za uchaguzi wa Shirikisho hilo.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF mwanzoni mwa juma hili ilitangaza kumpitisha Wallace Karia kuwa mgombea pekee wa kiti cha Urais, huku wapinzani wake wakienguliwa kwa kigezo cha kushindwa usahili.