Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewasimamisha kazi wahandisi watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupisha uchunguzi baada ya Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme Msamvu kuungua moto na kusababisha hasara ya takribani shilingi Bilioni 2.

Dkt. Kalemani ameyasema hayo, Mkoani Morogoro, Agosti 03, 2021 alipofanya ziara ya kukagua kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msamvu kilichoungua moto Agosti 2, 2021 baada ya kutokea hitilafu na kusababisha wananchi kukosa Umeme.

Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt.Tito Mwinuka pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Wizara na TANESCO.

Dkt. Kalemani amefafanua kuwa wahandisi hao wa TANESCO, wamesimamishwa kwa kushindwa kubaini hitilafu iliyotokea katika mifumo ya kuendeshea mitambo kituoni hapo, na kusababisha harasa kubwa kwa taifa baada ya kituo hicho kuungua moto.

Aidha amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mahimbali kuunda kamati ya kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha Moto huo na hasara iliyopatika ndani ya siku tano kuanzia leo Agosti 3, 2021.

Hata hivyo ameitaka TANESCO kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha umeme unarejea katika maeneo yote ndani ya saa 24 kuanzia leo,vilevile waongeze wataalam kutoka vituo vingine ili kuongeza nguvu kazi na kukamilisha kazi hiyo haraka.

Sambamba na hayo yote ameiagiza Kampuni ya inayotekeleza Mradi wa Reli ya Umeme (SGR) kumchungumza mhandisi wake anayedaiwa kusababisha hitilafu hiyo kwa kukata waya wa umeme na kari la kuchimbua barabara wakati akitekeleza majukumu yake na kuchukuliwa hatua pindi itakapobainika.

Wafugaji kunufaika na mbegu bora za mifugo ya asili
Peter Banda atua Msimbazi