Boniface Gideon – Tanga
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametangaza neema ya matibabu kwa baadhi ya Magonjwa yasiyoambukiza kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na maeneo jirani, huku wakitarajia kuzindua kambi maalumu ya kupima Afya bure na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata vipimo.
Waziri Ummy ameyasema hayo hii leo Agosti 14, 2023 na kudai kuwa kambi hiyo itakayofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia Augost 21 inatarajiwa kuwa na Wakazi zaidi ya 5000 watakaofanyiwa uchunguzi wa Magonjwa ya Kisukari, shinikizo la damu, Saratani ya tezi dume kifua kikuu, na magonjwa mengine yasiyoambukiza ikiwemo mlango wa kizazi na Malaria.
Amesema, “magonjwa yatayopimwa ni yale yanayoambukiza na yasiyoambukizwa na endapo mtu atakutwa na ugonjwa atapatiwa tiba lakini kwa wale ambao watakuwa na magonjwa kama yatahitaji upasuaji watapatiwa tiba watakapokuja Madaktari bingwa.”
“Takwimu inaonesha wapo watu laki mbili ambao hawajajitambua afya zao katika upimaji wa vvu, tunawashauri na kuwahamasisha watu kupima na kama watu wote ambao wana maambukizi wangekuwa wanafuata masharti ya kumeza dawa tunaweza kuutokomeza kabisa,” amesema Waziri Ummy.
Awali, Mratibu mkuu wa Afya check, Isack Maro alisema lengo la kuweka kambi mkoani hapa ni kutaka kuwajengea wananchi tabia ya kupima afya kwa hiyari mara kwa mara na hii ni mara baada ya kumaliza mkoani Dar es salaam ambapo zaidi ya wananchi 9324 walifanyiwa vipimo.
“Kitakwimu watanzania tunatumia gharama kubwa sana kujitibu kwa sababu tumechelewa kugundua tatizo, kampeni hizi zilianzishwa kuhakikisha kwamba watanzania wanajenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara,” alisema Maro.