Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambulika na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza kuwafukuza wabunge nane wa viti maalum na madiwani, Kambi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif imejibu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui amesema kuwa wanajipanga kufanya kikao vikao vya Kamati ya Utendaji na Baraza Kuu la chama hicho kujadili uamuzi uliotangazwa na Profesa Lipumba huku akidai kuwa ni uamuzi batili uliotokana na Baraza batili.
“Baraza Kuu halali la chama litatoa uamuzi wa nini muelekeo wa uamuzi uliotolewa na hawa watu ambao wengine tuliwasimamisha uanachama,” alisema Mazrui.
Julai 23 mwaka huu, Profesa Lipumba alitangaza uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho la kuwaondoa wabunge nane wa viti maalum kwa madai ya usaliti, hujuma na utovu wa nidhamu dhidi ya Mwenyekiti (yeye) na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Magdalena Sakaya.
- Mahakama Kuu yapigilia msumari malipo ya Bilioni 2 kwa AY na FA
- Video: Magufuli aibuka na Lissu, Mshtuko vyuo vikuu
Waliotajwa kufukuzwa ambao pia majina yao yaliwasilishwa kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ni pamoja na Riziki Ngwali, Severina Mwijage, Raisa Abdallah, Saumu Sakala, Salma Mwasa, Miza Bakari na Halima Mohamed, Khadija El Khasim.
Aidha, madiwani waliofutwa na uamuzi huo ni Leila Hussein na Elizabeth Magwaja, wote wa jijini Dar es Salaam.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema kuwa ofisi yake italitolea majibu suala hilo baada ya kufanya majadiliano.
Naye Spika Ndugai alikiri kupokea barua hiyo na kueleza kuwa bado anatafakari na atatoa maamuzi yake hapo baadaye.