Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) upande wa Bara anayetambulika na Ofisi ya Msajili wa VYama vya Siasa, Magdalena Sakaya amejibu mapigo baada ya mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea kutangaza jana ‘Oparesheni Ondoa Msaliti Buguruni’.
Kubenea alidai kuwa oparesheni hiyo inalenga kumuondoa katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Akijibu mpango huo uliotangazwa na Chadema inayomuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Sakaya ambaye ni kambi ya Profesa Lipumba alisema kuwa anawasikitikia Chadema kwa kuingilia mgogoro usiowahusu.
Sakaya aliongeza kuwa mpango huo wa Chadema hautafanikiwa kamwe na kwamba wanachokifanya ni ‘kushadadia’ yasiyowahusu. Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa kutokana na mpango huo, kambi yao pia itakuja na ‘Oparesheni Futa Chadema’.
“Tunasubiri watekeleze, hata sasa hivi tuko tayari. Ila wajue kuwa katika suala hili wao kama Chadema haliwahusu na kama haitoshi na sisi tutakuja na oparesheni futa Chadema,” Sakaya anakaririwa.
Katika hatua nyingine, Kubenea alipozungumzia majibu ya Sakaya alidai kuwa CUF ni sehemu ya Ukawa hivyo inapoonekana inataka kudhoofishwa ina maana kuwa Ukawa itadhoofika pia, hivyo hawako tayari kuliona hilo.
Kubenea alidai kuwa Profesa Lipumba anatumiwa kuidhoofisha CUF ambayo ni mshirika wake ndani ya Ukawa na kwamba hawatatumia nguvu kumuondoa bali watawahamasisha wanachama katika matawi yote kumkataa kidemokrasia.