Wakati harakati za kampeni nchini Kenya zikiendelea kushika kasi, kambi ya umoja wa vyama vya upinzani ya NASA imedai kuwa maisha ya mgombea wake wa urais, Raila Odinga na vigogo wengine wanne yako hatarini.
Madai hayo ya NASA yametolewa jana jijini Nairobi na Seneta wa Siaya, James Orengo wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alidai kuwa maafisa nane wa jeshi la polisi ambao wako kati ya kikosi maalum cha askari 60 waliopewa mafunzo ya kijeshi, wanamfuatilia kwa siri Odinga kwenye kampeni zake.
“Pia tuna taarifa kwamba kabla ya siku ya uchaguzi, idadi ya askari hao waliopewa mafunzo wamekuwa wakinyemelea mara kwa mara mikutano ya mgombea wa NASA, mheshimiwa Raila Odinga na viongozi wengine wa ngazi za juu,” Orengo anakaririwa na Citizen Kenya.
Aliongeza kuwa maafisa hao wamekuwa wakitumia magari maalum ambayo namba zake zimekuwa zikibadilishwa mara kwa mara.
NASA wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha usalama wa Odinga na viongozi wake, wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa nchi hiyo. Pia, wamelitaka jeshi la polisi nchini humo kutolea majibu madai hayo.
Kenya inatarajia kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8 mwaka huu, uchaguzi unaodaiwa kuwa wenye upinzani mkubwa zaidi katika historia ya chaguzi ngumu za nchi hiyo.
Kambi ya NASA imeendelea kuchuana na kambi ya JUBILEE. Matokeo ya tafiti zilizotolewa hivi karibuni yanampa nafasi zaidi mgombea wa JUBILEE, Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya mpinzani wake, Raila Odinga.