Mshambuliaji aliyetemwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mwishoni mwa msimu wa Ligi ya ‘PSL’ 2021/22, Lazarous Kambole ameshindwa kuficha siri ya wapi atakapocheza msimu ujao wa soka.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Zambia amejikuta akiweka wazi mpango wake wa Maisha, baada ya kuondoka Afrika Kusini, huku akiitaja Klabu ya Young Africans ambayo tayari imeanza usajili wa kuboresha kikosi chake, kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa.
Kambole amesema wakala wake kwa sasa yupo katika mazungumzo na Uongozi wa klabu hiyo ya Dar es salaam-Tanzania, na muelekeo wa kukamilika kwa makubaliano chanya upo vizuri.
Amesema lengo lake ni kuendelea kucheza soka la ushindani, na anaamini Young Africans ni mahala sahihi kwake, kutokana na klabu hiyo kuwa kwenye mkakati wa kufanya vyema katika Ligi ya Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa msimu ujao.
“Hapa tunavyozungumza nimekuja hospitali kumleta mtu, lakini kitu ambacho naweza kukwambia kwa sasa mambo yote yanakwenda sawa maana wakala ndiyo yupo katika kushughulikia vitu vya mwisho, hivyo ni jambo la kusubiria.”
“Siwezi kusema ni kwa muda gani wamekubaliana huo mkataba, niache kwa sasa halafu nitarejea kwako kukueleza kila kitu, lakini nakuja Young Africans,” amesema Kambole
Ikumbukwe hii siyo mara ya kwanza kwa Young Africans kumtaka mshambuliaji huyo ambapo msimu uliopita walishindwa kufikia muafaka kutokana na dau lake la usajili kuwa kubwa hali iliyofanya klabu hiyo ya Jangwani kukaa pembeni kabla ya kumrejea tena mwaka huu.