Kampuni inayojulikana kwa jina la ‘Blue Ivy’ inayomilikiwa na Veronica Morales imemtaka Beyonce kulipa $10 milioni ili atumie jina hilo kwenye biashara zake, jina ambalo ni la mwanaye mwenye umri wa miaka sita.
Kwa mujibu wa wanasheria wa Beyonce, walikutana na timu ya Morale ambaye ni mmiliki wa kampuni ya ‘Blue Ivy’ na kuzungumza nao lakini waliwataka kutoa kiasi hicho cha fedha, jambo ambalo walilikataa.
Timu hizo mbili zimefikishana mahakamani, baada ya Morale kumuwekea pingamizi Beyonce kutumia jina hilo kwa bidhaa za watoto na bidhaa za maharusi, biashara ambayo inaendana na biashara anayoifanya mwanamke huyo ikiwa na jina hilo.
Mwanasheria wa Beyonce ameeleza kuwa walikataa wazo hilo la Morales na kutaka waendelee na kesi yao kwani hawakutegemea kununua jina la mtoto wa Beyonce na Jay Z.
Morales alisajili kampuni yake kwa jina la ‘Blue Ivy’, Februari 8 mwaka 2012, mwezi mmoja tu baada ya Beyonce na Jay Z kumpata mtoto wao wa kike waliyemuita jina hilo.