Kaimu Afisa Habari wa klabu ya Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kuwa wanaoibeza TP Mazembe wakumbuke kuwa klabu hiyo ipo kwenye orodha ya vilabu 10 bora barani Afrika na inakuja kucheza na Simba ikiwa na kikosi bora.
Kamwaga ameyasema hayo baada ya kuwepo kwa maneno katika mitandao ya kijamii kuwa timu hiyo kwa sasa imeshuka na haipo vizuri.
Amesema ubora wa TP Mazembe haujawahi kushuka na wanaoibeza timu hiyo wana fikra potofu katika maendeleo ya soka la bara la Afrika.
“TP Mazembe bado ni klabu bora Afrika, inaendelea kuheshimika na haikuwa kusudi kwa uongozi wa Simba SC kuialika katika Tamasha la Simba Day, kuna kitu tumekiona ambacho kitaongeza morari kwenye maandalizi yetu ya msimu wa 2021/22.”
“Hao wanaobeza ninakuhakikishia watabadilika na kuandika mambo mengine ikitokea Simba imedroo ama kupoteza mchezo wa Simba Day, lakini kwa ubora wa kikosi chetu hatutapoteza hasilani.” amesema Kamwaga
Simba itavaana na TP Mazembe katika mchezo wa kirafiki Septemba 19, 2021 katika Tamasha la Simba Day litakalofanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.