Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Ezekiel Kamwaga amesema kikosi cha klabu hiyo hakitacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Young Africans, nchini Morocco.

Kamwaga ametoa ufafanuzi huo, kufuatia timu ya Simba kuweka kambi nchini Morocco tangu jana Jumatano (Agosti 11), huku Young Africans wakitarajiwa kuelekea nchini humo juma lijalo kuweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao 2021/22.

Baadhi ya wadau wa soka nchini kupitia mitandao ya kijamii, wametamani kuona manguli hao wa soka la Bongo wakicheza mchezo wa kirafiki nchini Morocco, kwa kuwa watakua sehemu moja kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.

Kamwaga amesema Simba SC haina Program yoyote ya kiufundi ya kucheza mchezo huo, zaidi ya kuheshimu misingi ya Program ya benchi la ufundi linaloongozwa na Didier Gomez.

“Hatuwezi kucheza na Young Africans mechi ya kirafiki nchini Morocco hata kama ni Pre Season” amesema Ezekiel Kamwaga

Hata hivyo mpaka sasa Uongozi wa Simba SC haujathibitisha kama kikosi chao kitacheza mchezo wowote wa kirafiki nchini Morocco, zaidi ya kuthibitisha tarehe ya Simba Day, ambayo itashuhudiwa mabingwa hao wakicheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Serikali kufufua vyuo vya ufundi
Droo ya Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho ni kesho