Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, umetangaza uhakika wa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kufika kwa wingi Uwanja wa Benjiamin Mkapa siku ya Jumapili (Septamba 19) kwa ajili ya Tamasha la Simba SC.
Akizungumza kwenye kipindi cha HQ kilichorushwa hewani leo Jumatano (Septamba 15) Kaimu Afisa Habari wa klabu ya Simba Ezekiel Kamwaga, amesema hawana shaka na Mashabiki na Wanachama wao kuhusu kufika Uwanjani siku hiyo.
Amesema imekua kawaida kwa wanasimba kufika kwa wingi Uwanjani, kwa ajili ya kufuatilia burudani ambazo kila mwaka zimekua zikiimarika katika Tamasha la Simba (Simba Day).
“Suala la kuujaza Uwanja sio la kuuliza kwa Simba SC, mashabiki na wanachama wa Simba wanaipenda timu yao na Simba Day kwao ni sehemu ya sherehe yao kwa kila mwaka, watafika kwa wingi na kudhihirisha hilo kupitia televisheni za watu majumbani.”
“Simba imekua na kawaida ya kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa tangu enzi na enzi, kwa hiyo hilo sio suala la kutupa wasiwasi sisi viongozi ambao tumewaandalia mashabiki na wanachama wetu vitu vuzuri katika tamasha lao ambalo kila mwaka limekua na ladha mpya.” amesema Ezekiel Kamwaga
Tamasha la Simba Day hutumika kuwatambulisha wachezaji waliosajiliwa Simba SC kwa msimu husika, sambamba na kutoa burudani mbalimbali pamoja na mchezo wa kimataifa wa kirafiki ambapo mwaka huu Mabingwa wa Tanzania Bara watacheza dhidi ya Mabingwa mara tano wa Afrika TP Mazembe.