Bondia wa ngumi za kulipwa kutoka nchini Malawi, Israel Kamwamba ameanza kuchimba mikwara mapema kwa kumwambia mpinzani wake, Loren Japhet wa Tanzania kuwa anakuja nchini kwa kazi moja ya kumaliza utawala wake.
Kamwamba ametoa vitisho hivyo kuelekea katika pambano la Kivumbi Dodoma linalotarajia kupigwa Juni 24, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Chinangale Park jijini Dodoma ambapo Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’ atapanda ulingoni dhidi ya Charles Misanjo wa Malawi.
Kamwamba amesema mipango yake kwa sasa ni kuhakikisha anakuja nchini kupoteza utawala wa Loren Japhet Kutokana na maandalizi makali anayoendelea kufanya nchini kwao.
“Loren nataka nikwambie kwamba nakuja Tanzania kwa kazi moja ya kuhakikisha napiga kipigo kibaya ambacho nitamaliza utawala wako kwa sababu nafahamu vizuri juu ya ubora wako hivyo hautoweza kunisumbua kazi yangu itakuwa ya kutisha juu yako maana nataka nikupige kwa KO mbaya.
“Nataka ujue kwamba siyo mgeni na Tanzania kwa sababu nimeshakuja sana kupigana hivyo hauna jambo lolote la kunieleza zaidi ya kukupa kichapo kizito, najua wewe ni bondia mzuri ila mimi ni mzuri zaidi yako nawashukuru sana Mitra Boxing Promotion kwa nipa kazi hii ambayo itakuwa mbaya kwako,” amesema Kamwamba
Lakini kwa upande wa mratibu wa pambano hilo kutoka Mitra Boxing Promotion Chubert Mwarabu amesema kuwa: “Mitra Boxing Promotion tumeichagua Dodoma katika pambano letu linalotarajia kupigwa Juni 24, mwaka huu ambapo bondia wetu, Mtanzania mwenzetu Karim Mandonga atapanda ulingoni dhidi ya Charles Misanjo kutoka Malawi, litakuwa ni pambano la kipekee kutokana na fursa zilizopo hapa Dodoma na nguvu ya serikali yenyewe ipo hapa Dodoma.”