Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kinatarajiwa kwenda Tanga keshokutwa Jumatatu kwa ajili ya michuano ya Ngao ya Jamii huku benchi la ufundi likiweka wazi wanafuata ubingwa wa michuano hiyo.
Young Africans ambayo imetwaa Ngao ya Jamii mara mbili mfululizo wakiifunga Simba SC, itafungua michuano hiyo kwa kucheza dhidi ya Azam FC Jumatano, katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Afisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe amesema kikosi chao kitaondoka Jumatatu kwa usafiri wa ndege.
“Kikosi kitaelekea Tanga Jumatatu, tutakuwa na siku moja ya mazoezi siku ya Jumanne na Jumatano ndiyo tutacheza pambano letu dhidi ya Azam FC” amesema Kamwe.
Kamwe amesema benchi la ufundi chini ya kocha Miguel Gamondi amewahakikishia wanaenda kufuata taji hilo la Ngao ya Jamii na kurudi nayo Dar es salaam.
“Kila kitu kipo sawa, benchi la ufundi limetuambia kikosi kipo tayari sasa kuifuata ngao yetu, tunaenda Tanga kuendeleza furaha yetu pale tulipoishia msimu uliopita,” amesema Kamwe.
Aidha, amewataka Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo mikoa ya Pwani, Kilimanjaro na Arusha kufurika kwa wingi Uwajani ili kuwapa hamasa wachezaji ambao watakuwa wanaanza kazi ya kutetea mataji yao waliyoyapata msimu uliopita.
“Niwaambie Wanachama na Mashabiki wa Young Africans wa mikoa ya jirani na Tanga wajitokeze kwa wingi, Jumatano ni siku yetu ya kwenda kuujaza Uwanja wa Mkwakwani, waje wawape sapoti wachezaji wao,” amesema Kamwe.
Wakati Young Africans ikijiandaa kucheza dhidi ya Azam FC, mchezo mwingine wa Ngao ya Jamii utakuwa kati ya Simba SC dhidi ya Singida Fountain Gate, utakaopigwa Alhamis (Agosti 10) Uwanja wa CCM Mkwakwani. Mshindi wa kila mchezo watakutana kwenye Fainali kuwania tají hilo kwa msimu huu 2023/24.