Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa Young Africans Ally Kamwe, ameweka wazi kuwa, wapinzani wao kutoka nchini Misri Al Ahly, watakutana na muziki kamili kutokana na wachezaji wote kuwa fiti.
Young Africans inayonolewa na Kocha kutoka nchini Argentina Miguel Gamondi, itakuwa na kibarua cha kusaka alama tatu kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi D dhidi ya Al Ahly unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam keshokutwa Jumamosi (Desemba 02).
Kamwe amesema:”Ni mchezo mgumu ambao utakuwa na ushindani mkubwa, lakini uzuri ni kwamba kila mchezaji yupo tayari kwa ajili ya mchezo huo, hivyo wapinzani wetu watakutana na muziki uliokamilika. Hawataamini macho yao baada ya dakika tisini.
“Tutakuwa nyumbani mbele ya Wanachama na Mashabiki wetu, hivyo ni muda sasa kuelekea kupata burudani kwenye mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya kupoteza mchezo wa kwanza. Yale yaliyopita tumesahau, tunasonga mbele.”
Mchezo uliopita wa Kundi D, Young Africans ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad ikiwa ugenini nchini Algeria. Huu unatarajiwa kuwa mchezo wa kwanza hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa nyumbani.