Kanisa la Anglikana nchini Kenya limepiga marufuku michango inayotolewa na wanasiasa nchini humo kuunga mkono huduma mbalimbali kanisani.
Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Jackson Ole Sapit ametangaza marufuku hiyo akieleza kuwa kanisa litapokea sadaka kutoka kwa kila mtu lakini sio michango ya wanasiasa.
Akizungumza jana katika Kaunti ya Kiambu, Askofu Mkuu Sapit alitoa wito kwa makanisa yote kukataa michango ya wanasiasa ili wasitumie madhabahu kufanikisha ajenda zao za kisiasa.
“Hatutakubali kuwaacha watu watumie madhabahu kama sehemu ya kufanyia siasa, kama tunataka kukutana na Wakristo na kuwasalimia tunapaswa kufanya hayo nje ya kanisa. Na iwe kwamba kila saa ya ibada iwe saa ya ibada kweli ambapo kila tunachokisikia kiwe ni neno la Mungu na sio sera za wanasiasa,” alisema Askofu Sapit.
“Sadaka inapaswa kutolewa kwa siri kati yako na Mungu wako, sio kitu ambacho kinapaswa kuoneshwa… fanya hivyo kwa usiri haijalishi kiasi unachotoa. Lakini kama ni kwa ajili ya maonesho tunasema samahani kwa sababu kanisa halipo kwa ajili ya maonesho,” aliongeza.
Awali, Mkurugenzi wa Mashtaka, Noordin Haji aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha kuwa hawapokei michango ambayo inatokana na fedha zenye utata.
Alieleza kuwa wachangiaji wa mamilioni wakati mwingine hufanya hivyo kwa lengo la kutakatisha fedha zilizopatikana kwa njia chafu.