Kiungo Mkabaji kutoka nchini Mali na klabu ya Simba SC, Sadio Kanoute amevutiwa na taarifa za klabu hiyo kuwa mbioni kumsajili Kiungo wa Red Arrows ya Zambia Allasane Diarra.
Kanoute ambaye ameitumikia Simba SC msimu huu 2021/22 akitokea Al Ahly SC Benghazi ya Libya, amesema amesikia taarifa za usajili wa kiungo huyo kutoka Mali, na anaamini kama atafanikisha dili lake la kutua Msimbazi basi mambo yatakua Bam Bam.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 amesema, aliwahi kucheza na Diarra kwenye Ligi Kuu ya nchini kwao Mali pamoja na timu ya taifa ya vijana, hivyo anafahamu uwezo wake wa kupambana.
“Sina shaka na Diarra naamini katika uwezo wake ni moja ya viungo wazuri washambuliaji ila kama kuna jambo lingine lolote sifahamu kwa maana sina mawasiliano nae ya mara kwa mara,” amesema Sadio.
Simba SC inatajwa kuwa kwenye mpango wa kumnasa Diarra, kufuatia kuridhishwa na uwezo wake kisoka, na tayari aliwahi kucheza dhidi ya wababe hao wa Msimbazi katika mchezo wa Mchujo wa Kombe la Shirikisho jijini Dar es salaam (Tanzania) na Lusaka (Zambia) mwishoni mwa mwaka 2021.
Usajili wa kiungo huyo unatajwa kuwa sehemu ya mapendekezo yaliyoachwa na Kocha Pablo Franco Martin, ambaye mwanzoni mwa juma lililopita alivunjia mkataba wake, kwa kigezo cha kushindwa kufikia malengo aliyowekewa na Uongozi wa Simba SC.
Pablo alipendekeza usajili wa kiungo kiungo mshambuliaji mmoja wa kigeni, kupitia ripoti yake ambayo aliiwasilisha kwa viongozi, kabla ya kuondoka nchini.
Hata hivyo imeelezwa kuwa jina la Diara limepitishwa na viongozi wa Simba SC, baada ya mchakato wa kupitia majina mengine ya viungo washambuliaji wanne, ambao walipendekezwa kusajiliwa klabuni hapo.
Viongo wengine ambao walijadiliwa na jopo la viongozi wa Simba SC ni Victorien Adebayor anayehusishwa na mpango wa kusajiliwa na Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika RS Berkane ya Morocco, Morlaye Sylla na Stephane Aziz Ki anayehusishwa na Young Africans.